Mbunge wa Jimbo la Ubungo-Chadema, Mh John Mnyika
---
Shirika la Umeme (TANESCO) linakabiliwa na ufisadi
na uzembe unaoongeza gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme
kwa upande mmoja na uendeshaji wa shirika kwa upande mwingine. Ufisadi na uzembe huo unapunguza uwezo wa
TANESCO kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na unaongeza gharama na bei
ya upatikanaji wa umeme hali inayoathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi
kwa kuchangia katika mfumuko wa bei na ongezeko la gharama za maisha. Mzigo wa
ufisadi na uzembe katika TANESCO unajitokeza zaidi katika mikataba mibovu
pamoja na ukiukwaji wa sheria za ununuzi wa umma, ubadhirifu na matumizi mabaya
ya madaraka.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ibara ya 63 sehemu ya pili ya bunge (inayoundwa na wabunge) ndio
chombo kikuu chenye madaraka na mamlaka kwa niaba ya wananchi ya kuisimamia
serikali. Hata hivyo, katika kipindi cha kati mwaka 2008 mpaka 2012 maazimio ya
Bunge kuhusu sekta ya nishati ikiwemo kuhusu umeme yamekuwa hayatekelezwi kwa
wakati na kwa ukamilifu hali inayofanya tuhuma za ufisadi na uzembe kuendelea
kujirudiarudia. Katika muktadha huo, ni muhimu kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba ya
nchi ibara ya 8 madaraka na mamlaka ni ya umma (serikali inafanya kazi kwa
niaba tu) ipo haja ya kuanza kuunganisha ‘nguvu ya umma’ katika kushinikiza
hatua kuchukuliwa kwa wahusika wa ufisadi na uzembe ili kuweka misingi bora ya
uwajibikaji katika sekta ya nishati.
Ili umma uweze kuungana kuchukua hatua ni muhimu
masuala yote ya ufisadi na uzembe yakaelezwa kwa uwazi kwa umma hivyo, katika
mfululizo huu nitaweka hadharani orodha za watuhumiwa wa ufisadi na uzembe
katika sekta ya nishati. Orodha hizi zinatolewa kwa awamu zikigusa kwa kuanzia
mashirika na taasisi zilizochini ya Wizara ya Nishati na Madini na baadaye
Wizara yenyewe na hatimaye Serikali kwa ujumla. Aidha, orodha hizi zitatolewa
kwa awamu masuala kwa masuala na matukio kwa matukio, ngazi kwa ngazi.
Katika orodha ya awamu ya kwanza nitaanza na TANESCO
kuhusu masuala na matukio yaliyohusu kampuni
ya M/S SANTA CLARA SUPPLIES COMPANY LIMITED pamoja na kampuni ya M/S McDONALD
LIVE LINE TECHNOLOGY LIMITED. Orodha nyingine zitafuata katika awamu ya baadaye
iwapo vyombo na mamlaka husika hazitachukua hatua ikiwemo juu ya tuhuma za
ufisadi na uzembe katika matumizi ya dola milioni 54 (zaidi ya bilioni 86)
katika ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL.
Bonyeza
hapa kusoma ORODHA
YA KWANZA YA WATUHUMIWA WA UFISADI NA UZEMBE KATIKA SHIRIKA LA UMEME (TANESCO)
Nimetoa
majina haya hadharani ili umma uunganishe nguvu kwa njia mbalimbali kutaka
hatua zichukuliwe dhidi ya ufisadi na uzembe ili kuhakikisha nchi inaongozwa
kwa utawala wa sheria na maadili katika utumishi wa umma.
Mamlaka
zinazopaswa kuchukua hatua ni pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sekretariati ya Maadili
ya Umma zote kila moja kwa nafasi yake zichunguze ukiukwaji wa sheria katika
masuala yaliyo kwenye majukumu yao na kuchukua hatua za ziada kwa kuzingatia
pia ripoti
ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo nimeitumia kama rejea
kwenye baadhi ya masuala katika orodha hii.
Aidha,
kwa kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeitisha
Mkutano wa Taftishi Juu ya Marekebisho ya Bei ya Umeme za TANESCO ambao
inakusudiwa bei ya umeme kupandishwa tena, ni muhimu masuala ya ufisadi na
uzembe ndani ya TANESCO yakajadiliwa kwa upana na umma, ili kupinga gharama
zinazotokana na hali hiyo zisiingizwe katika mahesabu ya kukokotoa bei.
Ikumbukwe
kwamba tarehe 9 Novemba 2011 EWURA ilipokea Ombi la Dharura toka TANESCO na
kupandisha bei kwa wastani wa asilimia 155 kuanzia tarehe 1 Januari 2012 na
niliunganisha umma kupinga na hatimaye EWURA ikapunguza asilimia hiyo na
kuruhusu nyongeza ya wastani wa asilimia 40.29 ambayo ndiyo inayotumika hivi sasa.
Hivyo,
nitumie nafasi hii kuhimiza pia umma kujitokeza tarehe 10 Disemba 2012 kuanzia
saa 4 asubuhi katika Ukumbi wa Karimjee Dar es salaam kwenda kutoa maoni kwa
kuzingatia Taarifa ya Gharama za Huduma ya Umeme (Cost of Service Study) na
zaidi kwa kupinga kuingizwa kwenye bei ya umeme gharama za uzembe na ufisadi
ili kupunguza athari katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi miaka 51 baada
ya Uhuru.
Wenu
katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
09/12/2012
ORODHA YA AWAMU YA KWANZA: JUU YA MASUALA NA MATUKIO YA UFISADI NA UZEMBE YALIYOHUSU MIKATABA YA MAKAMPUNI YA M/S SANTA CLARA SUPPLIES COMPANY LIMITED NA M/S McDONALD LIVE LINE TECHNOLOGY LIMITED.
Masuala
na matukio ya ufisadi na uzembe yaliyohusu mikataba ya makampuni ya M/s Santa
Clara Supplies Company Ltd na M/s McDonald Live Line Technology Limited ambayo
yamefanyika kinyume na sheria mbalimbali.
Kwa
ushahidi wa nyaraka baadhi ya sheria zilizokiukwa ni pamoja na Sheria ya
Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2004, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka
2004, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 na sheria nyinginezo.
Aidha, masuala na matukio ya ufisadi na uzembe katika mikataba hiyo yamefanyika
kinyume na kanuni, miongozo na maadili ya Shirika la Umeme (TANESCO).
Ufisadi
na uzembe umesababishwa na makosa mengine mbalimbali mathalani mgongano wa
kimaslahi, utovu wa uaminifu, matumizi mabaya ya ofisi na makosa mengine yaliyo
kinyume cha sheria na maadili ya viongozi na watumishi wa umma.
Orodha
ya wanaotuhumiwa kuhusika katika ufisadi na/ama uzembe huo 18 ni kama
ifuatavyo:
1. Mhandisi
WILLIAM GEOFREY MHANDO
Huyu
alikuwa ni mkurugenzi mkuu wa shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na ndiye
mtuhumiwa mkuu wa ufisadi unaohusu mikataba tajwa.
Akiwa
mkurugenzi mkuu wa TANESCO aliingia mkataba na kampuni ya SANTA CLARA kwa tenda
No PA/001/11/HQ/G/011 kuleta vifaa vya ofisini, kwa kipindi hicho kampuni hiyo
tajwa hapo juu ilikuwa inamilikiwa na wanahisa ambao ni familia ya Mhando
mwenyewe.
Mkataba
huo ulisainiwa na mkewe kama mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo ya CLARA, kitendo
hicho cha mkurugenzi kuipatia kampuni ya mkewe tenda ni kinyume na maadili ya
Tanesco kifungu cha 2.2, ni kinyume na Sheria ya Ununuzi ya umma kifungu cha
33, 73(3) na 73 (5) pamoja na sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu cha
6 (d), (e) kutokana na kuwa na mgongano wa maslahi na utovu wa uaminifu.
Aidha
kusaini kwa mkataba huo yeye akiwa mkurugenzi wa TANESCO ni matumizi mabaya ya
ofisi, kwa kutumia ofisi ya umma kujinufaisha yeye pamoja na familia yake na
kushindwa kusimamia sheria zinazoongoza na kusimamia ununuzi wa umma.
Kwa
upande mwingine, aliingia katika makubaliano na Donald George Mwakamele
(mkurugenzi na mwanahisa katika kampuni ya McDONALD) makubaliano ambayo hayaruhusiwi na yenye
mgogoro ( Conflicting Joint Venture Agrement) kinyume na maadili ya TANESCO na
sheria nyingine za nchi nilizozitaja awali.
Lakini
pia akijifanya ni mfanya biashara alisaini na makubaliano na kampuni hiyo
makubaliano ya pande mbili ya kutafuta tenda, kununua, kujenga, kufanya
matengenezo na kufanya miradi yote inayohusika na umeme. Katika kuwezesha hilo
Mhando alikuwa na jukumu la kutafuta miradi ya umeme na endapo ikikamilika
pande hizi mbili zinagawana mapato na faida inayotokana na miradi hiyo wakati
huo huo yeye akiwa mtumishi wa TANESCO.
Pamoja
na kufukuzwa kazi, umma unapaswa kuunganisha nguvu kutaka Mhando achunguzwe kwa
makosa ya kijinai kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomhusu na kufunguliwa
mashtaka ya kukiuka sheria za nchi.
2. Bw.
HARUN MATTAMBO
Huyu
ni Afisa ugavi wa shirika la umeme Tanzania ( TANESCO) amefanya uzembe kwa
kushindwa kuhakikisha manunuzi yote yanayofanywa na shirika yanazingatia taratibu na kutimiza sheria za manunuzi ya
umma.
Aliruhusu
kufanyika kwa ufisadi na ukiukwaji wa sheria katika kupatikana kwa zabuni na.
PA/001/11/HQ/G/011 na kuathiri Shirika la Umeme (TANESCO).
Alipendekeza
kampuni ya M/s Mc Donald ipewe mkataba pamoja na kuwa haikuwa imetimiza
masharti ikiwemo kukwepa kuwasilisha mahesabu ya fedha yaliyokaguliwa ya mwaka
2009 kama sheria ilivyohitaji.
Matokeo
ya uzembe wake wa kuruhusu ufisadi ni kulisababishia hasara Shirika la Umeme
(TANESCO) kwa kuwa kampuni hiyo ya Mc Donald ilipatikana bila kushindanishwa na
makampuni mengine yaliyokuwa na unafuu na yaliyotimiza masharti.
Umma
uungane kutaka Matambo afukuzwe kazi mara moja, na kuchunguzwa kuhusu tuhuma za
kufanya uzembe huo kwa lengo la kujinufaisha na kunufaisha washirika wake kwa
ajili ya hatua za ziada za kisheria.
3. Bw ROBERT SHEMHILU
Huyu
aliwahi kuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa TANESCO na anatuhumiwa kufanya uzembe
ulioruhusu ufisadi.
Alifanya
makosa ya kuruhusu malipo yaliyofanyika tarehe 5 Septemba 2011 kabla hata ya
kusainiwa kwa mkataba na kuruhusu kuletwa kwa vifaa kabla hata ya kusainiwa kwa
mkataba katika ya TANESCO na kampuni iliyopewa kinyemela zabuni ya kuleta
vifaa.
Alifanya
pia makosa ya kuilipa kampuni ya Mc Donald malipo ya juu ya asilimia 30 ya
thamani ya mkataba wakati vifungu vya 26 na 54.1 vya mkataba huo (pamoja na
kuingiwa kinyemela) vilielekeza malipo ya asilimia 15 tu.
Shemhilu
pamoja na kusimamishwa umma uunganishe
nguvu kutaka, afukuzwe kazi mara moja na kuchunguzwa kwa ajili ya hatua za
ziada.
4. FRANCE
MCHALANGE, NAFTARI KISIGA NA SOPHIA MSIDAI
Hawa walifanya uzembe wa kushindwa kusimamia Sheria ya
Ununuzi wa Umma pamoja na maadili kwa kupendekeza kwamba Kampuni ya SANTA CLARA
ipewe zabuni ya kuuzia vifaa TANESCO pamoja na kufahamu kuwa kampuni tajwa
ilikuwa haijatimiza masharti na kulikuwa na mgongano wa maslahi.
Umma uhakikishe wanachukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na
kukiuka sheria ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wa umma kuwajibika kutoa
mapendekezo kwa kuzingatia sheria na maslahi ya umma.
5.
Mhandisi DECLAIN MHAIKI na Bw SUKE
Akiwa mtumishi wa umma alizembea na kukwepa kutoa
taarifa kuhusu kukiukwa kwa vigezo na
masharti kuhusu zabuni na. PA/001/09/HQ/W/014 na kufanya kampuni ya McDonald
Live Line Technology ipatiwe zabuni kinyume cha sheria ya ununuzi wa umma ya
mwaka 2004.
Aidha alichangia kufanya kampuni hiyo kupewa zabuni pamoja
na kuwa haikuwa na uwezo wa kifedha na kuiwezesha kupewa malipo ya asilimia ya
ziada kinyume na mkataba. Huyu naye umma uhakikishe wanachukuliwa hatua za
kinidhamu kutokana na kukiuka sheria na mkataba.
6. Mhandisi
D. MHAIKI, S.NKONDOLA, N.NTIMBA.Mhandisi CHEGERE, MAKIA NA MWITA.
Wote
kama timu walifanya maamuzi yaliyosababisha kutolewa kwa mkataba na.
PA/001/HQ/W/14 wa tarehe 11 Machi 2010 kwa kampuni ya Ms. Donald Live Line
Technology bila kuzingatia uwezo wa kitaalamu, kifedha na masharti mengine na
hivyo kukiuka sheria ya ununuzi ya umma na kushindwa kulinda maslahi ya taifa.
Hawa wanapaswa kuchukuliwa hatua za kinadhamu ili kudhibiti
maamuzi na mapendekezo ya wataalamu katika utumishi wa umma kuingiza mashirika
ya umma na nchi katika mikataba mibovu ili kupanua wigo wa uwajibikaji.
7.
FATUMA CHUNGU, ATHANASIUS NANGALI,
ELANGWA MGENI
Kundi hili limehusika katika majadiliano na kutoa
mapendekezo yaliyowezesha kampuni ya McDonald kupewa mkataba kinyemela.
Iwapo kundi hili lisingefanya uzembe na kusababisha
ukiukwaji wa sheria mchakato wa mkataba huo kati ya mwezi Machi mpaka Mei 2009
ungewezesha TANESCO kuingia mkataba na kampuni yenye uwezo na iliyotimiza
masharti na kuepusha shirika hilo kupata hasara na kubeba gharama ambazo
zingeweza kuepukika.
Ni muhimu wakachukuliwa hatua za kinadhamu ikiwa ni sehemu
ya kuchangia katika kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwa umakini na
ueledi ili kuepusha TANESCO kuendelea kufanya majadiliano na kuingia mikataba
mingine mibovu yenye kuongeza mzigo wa gharama kwa shirika na hatimaye ongezo
la bei kwa wananchi.
8.
LUSEKELO KASSANGA (MKURUGENZI WA
FEDHA)
Huyu alibariki ufisadi wa malipo yenye mkanganyiko katika
TANESCO kwa kuilipa kampuni ya Santa Clara mapema kabla hata haijafanyiwa
tathmini na kupatiwa zabuni.
Malipo yalifanyika kinyemela tarehe 5 Septemba 2011 wakati
ambapo tathmini ya zabuni ilifanyika tarehe 23 Septemba 2011, maana yake ni
kwamba malipo yalifanywa kabla hata kampuni husika haijapewa kazi kwa mleta
vifaa asiye na uwezo na mwenye mgongano wa kimaslahi.
Kassanga anapaswa kufukuzwa kazi na kuchunguzwa kuhusu
tuhuma za ziada za kunufaika kutokana na baadhi ya malipo yaliyofanywa kwa
makampuni mbalimbali wakati akiwa mkurugenzi wa fedha ili aweze kuchukuliwa
hatua zaidi za kisheria.
Sunday, December 9, 2012
Maadhimisho ya Miaka 51 ya Uhuru: Uwajibikaji, Uadilifu na Uzalendo ni nguzo ya Maendeleo ya Taifa
Leo
ni kumbukumbu ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania Bara),
maadhimisho yanayoendelea yamenifanya nikumbuke, waraka niliouandika mwaka 2011
(“Uhuru na Mabadiliko”) wakati wa kumbukumbu ya miaka 50 ya Uhuru wa
Tanganyika.
Kwamba
“Ili uhuru wetu uweze kuwa wenye matokeo kwenye maisha yetu na ya taifa letu
tunahitaji kuungana kufanya mabadiliko ya kweli. Changamoto kubwa ambayo
nimeiona ni kwamba kuna udhaifu katika mifumo yetu ya kiserikali kwenye ngazi
mbalimbali hali ambayo inakwaza hatua za haraka za kuleta mabadiliko.
Kwa
pamoja tunapaswa kuendelea kulitoa taifa letu katika kufilisika kimaadili na
kiitikadi na kukubaliana tunu za kitaifa zenye kuwezesha misingi ya
uwajibikaji. Uhuru wa kweli wa kisiasa utakuja kwa kuwa na uongozi wenye maono
(vision) na maadili (values) na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya
kiuchumi na kijamii katika kipindi cha kuanzia sasa na kuendelea kutuwezesha kunufaika
na rasilimali zetu: iwe ni vipaji vyetu, kodi zetu au maliasili za nchi yetu.”.
Maudhui
ya waraka huo unaopatikana kupitia http://mnyika.blogspot.com/2011/12/waraka-wa-pili-wa-mbunge-kwa-wananchi.html
au http://xa.yimg.com/kq/groups/20674633/136049788/name/Waraka+wa+John+Mnyika.pdf
Mara
baada ya maadhimisho yanayoendelea katika Uwanja wa Taifa, nitakuwa kwenye
mitaa mbalimbali ya kata ya Ubungo kwenye mikutano na wananchi tukitafakari
kuhusu nchi yetu na kuhamasisha umma kuunganisha nguvu kuchukua hatua dhidi ya
ufisadi na uzembe katika muktadha wa kauli mbinu ya Maadhimisho ya Miaka 51 ya
Uhuru iliyotolewa na Serikali mwaka huu wa 2012 ‘Uwajibikaji, Uadilifu na Uzalendo ni nguzo ya Maendeleo ya Taifa’.
Lengo
likiwa kuendelea kuunga mkono vuguvugu la mabadiliko kwa ajili ya kuleta
uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa
maendeleo endelevu ya Jimbo letu na Taifa letu kwa ujumla.
Nawatakia upendo, furaha na mafanikio katika kumbukumbu ya uhuru huku tukiweka
mstari wa mbele ukweli, uadilifu, na uwajibikaji katika maisha yetu.
No comments:
Post a Comment