Taswira Za Wanajeshi Watatu Waliohukumiwa Kunyongwa Hadi Kufa Wakiwa Mahakama Kuu ya Dar es Salaam baada ya kupatikana na hatia ya Kumuua Swetu Fundikira
Askari
watatu wakiwa kizimbani katika Mahakama Kuu ya Dar es Salaam jana ambapo
mahakama hiyo imewahukumu kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya
kumuua Swetu Fundikira, mtoto wa mdogo wa mwanasiasa maarufu nchini Chifu
Abdallah Fundikira. Kuanzia kulia ni Sajent Roda Roberth, Koplo Ally Ng’umbe na
Koplo Mohamed Ally. Picha na Venance Nestory --
Jaji Zainabu Muruke:“Hivyo mahakama hii inatamka kuwa
mshtakiwa wa kwanza, mshtakiwa wa pili na mshtakiwa wa tatu mmepewa adhabu ya
kifo, mtanyongwa hadi kufa.”
--
Na James Magai
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewahukumu adhabu ya
kunyongwa hadi kufa askari watatu baada ya kupatikana na hatia ya kumuua, Swetu
Fundikira.Adhabu hiyo ilitolewa jana na Jaji Zainabu Muruke baada ya
kuwatia hatiani wanajeshi hao kwa kosa la kumuua kwa makusudi Fundikira, kinyume
cha kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu.MT 1900 Sajenti Roda Robert (42)
na MT 85067 Koplo Mohamed Rashid wote wa JKT Mbweni na MT 75854 Koplo Ally
Ngumbe (37) wa Kikosi cha JWTZ Kunduchi, walimpiga Fundikira, Januari 23 mwaka
huu saa 7:30 usiku wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na baadaye kufariki
dunia usiku huohuo wa kuamkia Januari 24, mwaka 2010, katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili. Hukumu hiyo ilifufua upya msiba
wa Swetu, baada ya ndugu zake kuangua vilio, huku chumba cha Mahakama kikigeuka
kwa muda kuwa sehemu ya msiba.Sambamba na vilio hivyo, ndugu
wawili wa marehemu Swetu walianguka chini na kuzirai kwa muda, kabla ya kupewa
huduma ya kwanza na kurejea katika hali ya kawaida.Akisoma
hukumu hiyo, Jaji Muruke alisema ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa
washtakiwa hao ndiyo waliomuua Fundikira, ushahidi uliotolewa na upande wa
Mashtaka (Jamhuri) ulikuwa ni ushahidi wa mazingira, kwamba Jamhuri imeweza
kuthibitisha mashtaka hayo.Alisema kuwa anakubaliana na
mtiririko wa ushahidi wa upande wa mashtaka kama ulivyoelezwa na mashahidi wake
sita akiwemo daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu pamoja na askari
polisi wawili ambao washtakiwa katika utetezi wao walishindwa
kuuvunja.“Sheria iko wazi ukiondoka na mtu au ukionekana naye kwa
mara ya mwisho na baadaye mtu huyo akapatikana na madhara, wewe ndiyo
unawajibika kutoa maelezo ya kina kuhusu yaliyompata mtu huyo,” alisema Jaji
Muruke na kuongeza;“Kisheria ukitoa maelezo ambayo
hayajakidhi haja na yana utata ni faida kwa upande wa mashtaka ambao hutegemea
ushahidi wa mazingira. Maelezo ya kina hayajatolewa na washtakiwa
wote.”Aliendelea, “Ushahidi wa Jamhuri japokuwa ni wa mazingira,
umejengwa thabiti na upande wa utetezi haukuweza kujenga matundu, ama kuuvunja
mnyororo huo, kidole kinawaelekea wao.”Jaji Muruke alisisitiza kuwa
katika kesi hiyo licha ya kuwa kuna ushahidi wa kimazingira, upande wa mashtaka
umeweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha mashaka.“Hivyo
kosa wanaloshtakiwa nalo limethibitishwa na Mahakama imewaona washtakiwa kuwa
wana hatia ya kumuua Swetu Abdallah Fundikira,” alisema Jaji Muruke, huku
akimuuliza wakili wa Serikali kama washtakiwa wana kumbukumbu zozote za makosa
ya jinai.Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi aliyejitambulisha
kwa jina moja la Kongola alijibu kuwa hakuna kumbukumbu za makosa ya jinai kwa
washtakiwa hao.Kabla ya kutoa adhabu hiyo Jaji Muruke alimpa nafasi wakili
wa washtakiwa hao, Karoli Muluge na washtakiwa wenyewe kusema lolote.Wakili
Muluge aliiomba Mahakama iwape adhabu ambayo ni nafuu kutokana na mazingira ya
kesi hiyo, kwamba umri wa washtakiwa ni mdogo, bado ni vijana ambao ni nguvukazi
ya Taifa na wanategemewa na familia zao.Mshtakiwa wa kwanza, Sajenti
Robert aliiomba Mahakama impunguzie adhabu akidai kuwa mama yake ni mjane na
anamtegemea na hakuna mtu mwingine wa kumsaidia, ana watoto wadogo na pia afya
yake siyo nzuri.Hata hivyo, Jaji Muruke alilazimika kumuamuru mshtakiwa wa
pili, Koplo Ngumbe kukaa chini baada kuanza kujitetea kuwa japo ametiwa hatiani,
hakuhusika na mauaji hayo.Kwa upande wake, mshtakiwa wa
tatu Koplo Rashid aliiomba mahakama imwonee huruma na impunguzie adhabu akidai
kuwa yeye bado ni mdogo na kwamba hilo ni kosa lake la kwanza.Baadaye
Jaji Muruke alisema kuwa ni kweli maombi ya mshtakiwa wa kwanza yanatia huruma
na kwamba mshtakiwa wa tatu hata kumbukumbu zinaonesha kuwa bado ni mdogo na
kwamba hilo ni kosa lake la kwanza, lakini pia kuna roho iliyopotea.“Kama
ilivyo ada, ni adhabu moja tu kwa mtu anayepatikana na hatia ya kuua kwa
kukusudia na hakuna mbadala.” alisema Jaji Muruke na kuongeza;“Hivyo
mahakama hii inatamka kuwa mshtakiwa wa kwanza, mshtakiwa wa pili na mshtakiwa
wa tatu mmepewa adhabu ya kifo, mtanyongwa hadi kufa.”Baada
ya kutamka adhabu hiyo Jaji Muruke alitoka katika chumba cha mahakama na ghafla
ndugu wa marehemu Fundikira walilipuka kwa vilio ndani ya Ukumbi wa Mahakama,
kama vile walikuwa msibani.Ndugu wawili wa marehemu, Mwasiti Fundikira
ambaye ni dada wa marehemu na Shelina Hamisi (mpwa wa marehemu) walianguka chini
na kuzirai kwa muda hali iliyowalazimu watu waliokuwa nao karibu kuwapatia
huduma ya kwanza hadi walipoanza kurejea katika hali zao za kawaida.Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Lucy ambaye
marehemu alimwacha akiwa na mimba, alisema kuwa alilia kwa sababu hakuamini kama
haki ingetendeka.Dada wa marehemu, Rehema Fundikira alisema kuwa alikuwa
akilia kwa uchungu kutokana na jinsi ndugu yao alivyouawa kinyama.Wakili
Muluge alisema hakuridhika na hukumu hiyo na kwamba atakata rufaa.Alisema
hakuna shahidi hata mmoja aliyewaona wakimuua na kwamba hata hayo majeraha
yaliyodaiwa kuwa ndiyo chanzo cha kifo cha Fundikira hakuna aliyeeleza jinsi
washtakiwa hao walivyoyasababisha, kama ni kwa kumpiga au kwa namna nyingine
yoyote.
No comments:
Post a Comment