Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, akitoa msimamo wa Tanzania kuhusu vitendo vya kikundi
cha waasi cha M23 kilichopo Mashariki mwa Congo DRC. Kushoto ni Balozi Simba
Yahya.
--
Mhe. Bernard K. Membe (Mb) (katikati) akilaani
mashambulizi ya kikundi cha waasi cha M23 kilichoteka mji wa Goma, Mashariki mwa
Congo DRC. Waziri Membe aliyasema hayo alipokuwa katika Mkutano na Waandishi
wa Habari uliofanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano, Wizara ya Mambo ya Nje,
mjini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. John M.
Haule na Kushoto ni Balozi Simba Yahya, Mkurugenzi wa Idara ya
Mashariki ya Kati, Wizarani.Picha na Tagie Daisy Mwakawago-Wizara ya
Mambo ya Nje
--
Na ALLY KONDO
SEIF
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Mhe. Bernard K. Membe (Mb) amelaani kitendo cha kikundi cha M23 kuteka mji wa
Goma na kutishia kuteka miji mingine ya Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC). Mhe. Waziri alitoa msimamo huo wakati alipozungumza na Waandishi wa
Habari jijini Dar es Salaam tarehe 22 Novemba, 2012.
Mhe. Waziri alisema kuwa hali ya usalama mjini Goma ni
mbaya kutokana na mashambulizi hayo ya M23 na hali hiyo ikiachwa iendelee,
Tanzania itaathirika kwa kiasi kikubwa kwani watu wengi watakimbilia hapa nchini
kama wakimbizi.
Aidha, Mhe. Waziri alisikitishwa na kikundi cha M23 cha
kupuuza wito uliotolewa na viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini
mwa Afrika (SADC) na Sekretarieti ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) wa kusitisha
mapigano hayo.
Mhe. Waziri aliendelea kueleza kuwa Tanzania
inasikitishwa na jeshi la Umoja wa Mataifa la MONUSCO lililopewa jukumu la
kulinda amani Mashariki ya DRC kwa kushindwa kuchukuwa hatua za kukomesha
mashambulizi hayo na badala yake kuwa mashuhuda wa mashambulizi yanayofanywa na
kikundi cha M23 dhidi ya Serikali na wananchi wa kawaida.
Aliuomba Umoja wa Mataifa utoe mamlaka ili MONUSCO iwe
na uwezo wa kisheria wa kukabiliana na waasi wa M23 kama sura ya 7 ya Umoja wa
Mataifa inavyoelekeza badala ya kutumia sura ya 6 ya Umoja wa Mataifa
inayosisitiza umuhimu wa kulinda amani bila kujibu
mashambulizi.
Kuhusu jitihada
zinazofanywa na SADC kwa kushirikiana na ICGLR za kutafuta suluhu ya kudumu ya
mgogoro huo, Mhe. Membe alisema kuwa mwezi Agosti, 2012 Wakuu wa Nchi wa Jumuiya
hizo walikutana mjini Kampala, Uganda na kuamua kuunda kikosi cha kulinda amani
ili kitumwe Mashariki ya DRC. Tanzania iliahidi kuchangia batalioni moja lakini
kikosi hicho cha kulinda amani hakijapata ridhaa ya Umoja wa
Mataifa.
Umoja wa Mataifa hautaki kutoa ridhaa ili kikosi hicho
kipelekwe DRC kwa hoja kuwa tayari jeshi la Umoja wa Mataifa lipo nchini
DRC.
Mhe. Waziri alihitimisha Mkutano wake kwa kutoa taarifa
kuwa nchi za SADC na ICGLR zitakuwa na mkutano nchini Uganda kuanzia siku ya
Ijumaa tarehe 23 Novemba, 2012 kujadili hatua za haraka za kuchukuwa ili
kukabiliana na mzozo wa DRC.
No comments:
Post a Comment