
KAULI YA VIJANA WA CHADEMA MKOA WA MWANZA
KWA nafasi yangu ya Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA)
Mkoa wa Mwanza, nimelazimika kutoa ufafanuzi na kuweka kumbukumbu sawa
na kutuliza munkari ya vijana wa mkoa huu na nchi nzima kutokana na
habari zilizosambazwa kwa njia mbalimbali za upashanaji habari.
Imeripotiwa katika njia hizo za upashanaji habari kuwa BAVICHA wanataka
Katibu Mkuu wetu wa Chama, Dkt. Willibrod Slaa, aondoke madarakani na
kwamba asipoondoka, wataandaa mandamano ya kumng’oa.
Napenda kutumia nafasi hii kusema maneno machache juu ya upuuzi huo
ambao kila mtu anajua umetokana, unaratibiwa na kusimamiwa na CCM, ikiwa
eti ndiyo moja ya mikakati ya Sekretarieti ya chama hicho inayoitwa
kuwa ni mpya.
Kwa nafasi yangu, mimi ndiye msemaji mkuu wa masuala yote yanayohusu
BAVICHA kwa mkoa wa Mwanza. Kwa mamlaka yangu ninaelewa fika vijana wa
Mwanza hawajawahi, wala hawana mpango wa kubeba propaganda za CCM dhidi
ya CHADEMA na viongozi wetu kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu, akiwemo
Katibu Mkuu, Dkt. Slaa.
Natumia fursa hii kuwaondolea wasiwasi vijana wa CHADEMA mahali kokote
ndani na nje ya nchi, vijana wa Mwanza tuko imara kukilinda chama chetu
na viongozi wetu dhidi ya propaganda za CCM na serikali ambazo zina
lengo ya kudhoofisha harakati za kujenga taasisi imara inayobeba
matumaini ya Watanzania kwa ajili ya ukombozi wa awamu ya pili.
Natumia nafasi hii pia kuwataka vijana wa CHADEMA Mkoa wa Mwanza
watulie, wakisubiri BAVICHA Mkoa ifanye maamuzi kwa kuzingatia maslahi
mapana ya umma wa Watanzania na chama chetu dhidi ya hila, njama na uchu
wa mtu mmoja mmoja miongoni mwetu ambaye anaamua ‘kufika bei’ na kubeba
propaganda za CCM.
No comments:
Post a Comment