Wednesday, November 14, 2012

RAIS ATOA SALAM ZA RAMBI RAMBI

Rambirambi za msiba wa MARIAM HAMISI

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahman Kinana kuomboleza kifo cha msanii wa Kikundi cha Sanaa cha Tanzania One Theatre (TOT), Ndugu Mariam Hamisi ambaye alifariki dunia alfajiri ya kuamkia jana, Jumanne, Novemba 13, 2012 mjini Dar es Salaam. TOT ni kikundi cha CCM.

Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Ndugu Kinana: “Nimepokea kwa masikitiko makubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Ndugu Mariam Hamisi ambaye  naambiwa kuwa amefariki dunia baada ya kujifungua mtoto. Ni taarifa zimenipa majonzi makubwa kwa sababu Ndugu Mariam Hamisi amepoteza maisha yake akiwa bado kijana sana. Ni jambo la kusikitisha vile vile kwamba Ndugu Mariam Hamis amepoteza maisha yake wakati akijaribu kumpa uhai binadamu mwingine kwa sababu uzazi siyo ugonjwa.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Katika uhai wake mfupi, Ndugu Mariam ametoa mchango mkubwa kwa chama chetu na nchi yetu kupitia sanaa. Tutaendelea kumkumbuka kwa uhodari wake wa kisanii na kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu na chama chetu kupitia nyanja ya sanaa.”

“Nakutumia wewe Ndugu Katibu Mkuu wa Chama chetu salamu zangu za rambirambi kufuatia kifo hiki. Aidha, kupitia kwako, natuma rambirambi za dhati ya moyo wangu kwa  wasanii wote wa TOT na wasanii wote nchini kwa kuondokewa na mwenzao, amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Vile vile napenda kupitia kwako kuwapa mkono wa pole nyingi wanafamilia ya Ndugu Mariam Hamis kwa kuondokewa na ndugu yao. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa. Naelewa machungu yao na naungana nao katika kuomboleza kifo hiki. Naungana nao pia kumwomba Mwenyeji Mungu, Mwingi wa Rehema, ilaze pema peponi roho ya Marehemu Mariam Hamisi. Amina.”

Rambirambi za msiba wa MBARUKU MWANDORO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitumia salamu za rambirambi familia ya Mzee Mbaruku Mwandoro kufuatia kifo cha mzee huyo kilichotokea alfajiri ya kuamkia leo, Jumanne, Novemba 13, 2012 kwenye Hospitali ya Hindu Mandal mjini Dar es Salaam.

Katika salamu zake, Rais Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kusikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee Mwandoro ambaye katika uhai wake aliutumikia umma wa Tanzania katika nafasi mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuwa Mbunge.

Amesema Rais Kikwete katika salamu hizo: “Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mzee Mbaruku Mwandoro. Mzee Mwandoro alikuwa mtumishi mzuri wa umma na katika nafasi zote alizopata kuzishikilia katika maisha yake alitumimkia kwa uhodai mkubwa akionyesha mapenzi makubwa kwa wananchi.”

“Nilimfahamu fika Mzee Mbaruku Mwandiro wakati wa uhai wake. Alikuwa mtu mwema na kiongozi hodari. Kifo chake kimetuondolea kisima cha busara ambacho tunakihitaji sana kwa wakati huu na katika mazingira ya sasa ya nchi yetu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Nawatumieni nyinyi wanafamilia salamu zangu za rambirambi kwa kuondokewa na kiongozi na mhimili wa familia yenu. Naelewa uchungu wenu katika kipindi cha sasa. Napenda kuwajulisheni kuwa niko nanyi katika kipindi hiki cha majonzi mkubwa. Namwomba Mwenyezi Mungu awape uvumilivu na subira katika wakati huu mgumu. Naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema poponi roho ya Marehemu Mzee Mbaruku Mwandoro. Amina

No comments:

Post a Comment